Dhana ya lugha

Kazi ya 1.1

Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Nataka nena na wewe, upate kunielewa,

Wengi washikwa kiwewe, kwa kushindwa nielewa,

Yapaswa unielewe, nimekwishakubaliwa,

Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.

Huwezi kuwazuia, waliokubaliana,

Mimi wananitumia, wapate kuelewana,

Kanuni wazingatia, ili kuwasiliana,

Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.

Mfumo wangu makini, sauti kupangilia,

Maneno kuyatumia, yenye mpango sawia,

Sentensi kuzitumia, mawazo kupangilia,

Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.

Maswali

  1. Mwandishi anazungumzia nini katika shairi hili ulilosoma?
  2. Ni nani waliokubaliana kuwasiliana kwa kutumia hicho alichokizungumzia mwandishi katika ubeti wa pili wa shairi?
  3. Ni mambo gani matatu yaliyojumuisha na mwandishi katika katika mfumo wa jambo alilozungumzia?
  4. Unafikiri kwa nini mstari wa mwisho wa kila ubeti umerudiwarudiwa na mwandishi katika shairi hilo?

Kazi ya 1.2

Maneno yafuatayo yameandikwa kwa kuchanganya herufi. Chunguza maneno hayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

  1. Luagh
  2. anomasiliwali
  3. unabidam
  4. ribaha

Maswali

  1. Je, maneno hayo yana makosa gani?
  2. Kuna changamoto gani katika kusoma maneno hayo?
  3. Nini kifanyike ili maneno hayo yaweze kusomeka vizuri na kuleta maana?
  4. Andika maneno hayo kwa usahihi.
  5. Kutokana na uelewa ulioupata, lugha ufasiliwaje?

Zingatia

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimebuniwa na kukubaliwa na jamii ya watu ili zitumike katika mawasiliano baina yao. Mfumo huo hujumuisha sauti, silabi, neno, na sentensi. Ili watu au jamii iweze kuwasiliana, sharti lugha inayotumika iwe inaeleweka vizuri kwa kuwa lugha ni chombo cha mawasiliano. Unapowasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili ni muhimu kuzingatia kiimbo, mkazo, matamshi na lafudhi sahihi.

Post a comment

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *